Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania

TLSB Logo TLSB Logo
Tafuta kwenye kwa

Kongamano la Taifa

Kongamano la Kwanza la Huduma za Maktaba Tanzania na Tamasha la Vitabu na Usomaji lilizinduliwa rasmi mnamo mwezi Novemba mwaka 2021 na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mh. Juma Omar Kipanga (MB).

Kongamano hili na Tamasha la Vitabu liliandaliwa na Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) kwa Udhamini Mkubwa wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kufanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, Dodoma kuanzia tarehe 15 hadi 17 Novemba 2021.

Lengo kuu la Kongamano na Tamasha ilikuwa ni kutoa fursa kwa wadau wote wa Huduma za Maktaba nchini kushiriki, kuchangia na kuamua kwa pamoja namna bora ya kuendesha Huduma za Maktaba nchini kwa maslahi mapana ya Taifa.

Pamoja na mambo mengine, Kongamano lilitazama namna matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kuandaa, kukusanya, kuchakata, kuhifadhi na kusambaza taarifa inavyoweza kuwa chachu ya mageuzi makubwa ya uboreshaji wa Huduma za Maktaba nchini.

Malengo mahususi ya kongamano na Tamasha yalikuwa ni kutoa elimu kwa wasomaji na wananchi kwa ujumla kuhusu Huduma za Maktaba zitolewazo na Bodi katika Maktaba ya Taifa, Maktaba za Mikoa, Wilaya na Tarafa, na kutambulisha huduma za maktaba zilizoko mashuleni, vyuoni, na kwenye taasisi mbalimbali za mafunzo na utafiti; ili kujenga ufahamu na kuongeza matumizi ya huduma hizi kwa maendeleo endelevu ya nchi na watu binafsi; Kuelimisha na kushirikisha jamii kuhusu mikakati iliyopo ya kuboresha Huduma za Maktaba nchini; Kurahisisha upatikanaji, uhifadhi na usambazaji wa habari na taarifa sahihi kupitia vitabu, majarida, magazeti vilivyomo maktaba kwa wakati ili kukuza tabia ya usomaji; na Kuelimisha jamii kuhusu fursa zipatikanazo ndani ya maktaba.

Kongamano lilikuwa na matukio mbalimbali kama vile; Sherehe za Ufunguzi rasmi wa Kongamano; Uzinduzi wa Vitabu; Uwasilishaji wa Mada mbalimbali; Washiriki kutembelea Tamasha la Maonyesho ya Vitabu; Majadiliano ya Mada mbalimbali; Kupokea Maoni na Mapendekezo ya Wadau kuhusu Mada zilizotolewa; Kupitisha Maazimio ya Kongamano la Huduma za Maktaba Tanzania; Utoaji wa Tuzo na Zawadi; Kufunga Kongamano; na Washiriki Kutembelea Maktaba ya Bunge la Tanzania, Dodoma.

Maazimio ishirini (20) yaliafikwa katika kongamano hilo kwa ajili ya utekelezaji na mrejesho wa maazimio hayo utaletwa katika kongamano la mwaka huu hapo mwezi Novemba 2022.

Kongamano lilifungwa tarehe 17 Novemba, 2021 na Mgeni rasmi Mhe. Jabir Shekimweri, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, akimwakilisha Mhe. Anthony Mtaka, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.

Katika Sherehe hizo za kufunga, Mgeni rasmi alikabidhi Tuzo mbalimbali ikiwemo Tuzo ya Heshima kwa familia ya Ezekiel E. Kaungamno aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kwanza Mzawa wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania. Hii ilikuwa ni kutambua na kuenzi mchango wake katika kuboresha na kuendeleza huduma za Maktaba na Taaluma ya Ukutubi Tanzania.

Halikadhalika Mgeni rasmi alizitunuku vyeti Taasisi zote zilizoshiriki Kongamano hili la kihistoria. Aidha, wawasilishaji wote wa Mada walipewa vyeti kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuandaa na kuwasilisha Mada. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilipewa zawadi maalumu kwa kudhamini kongamano.