NAIBU KATIBU MKUU (ELIMU) WyEST AFANYA ZIARA TLSB
04 Aug, 2025
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Hussein Mohamed Omar ametembelea Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) Makao Makuu Dar es Salaam leo tarehe 22 Julai, 2025 kujionea na kujifunza shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Bodi ikiwa ni takribani mwezi mmoja sasa tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo.
Dkt. Omar, amesema lengo la ziara hiyo ni kuifahamu TLSB na shughuli zake huku akitumia fursa hiyo kuipongeza Bodi kwa hatua iliyofikia kuelekea utoaji wa huduma za Maktaba kwa njia ya Mtandao kupitia Maktaba Mtandao Jumuishi ya Kitaifa ambayo iko mbioni kuzinduliwa.
"Nitumie fursa hii kuwapongeza sana Bodi na Menejimenti kwa hatua mliyofikia kuelekea kutoa huduma za Maktaba kidijitali, hatua hii itawezesha wananchi walio wengi hasa waishio pembezoni mwa miji kupata huduma za maktaba kwa urahisi na kuchochea utamaduni wa kujisomea na kujipatia maarifa” amesema Dkt. Omar.
Sambamba na hilo, ameongeza kuwa atafanya jitihada za kutafuta washirika na miradi itakayowezesha Watumishi wa Bodi kwenda kujifunza nje ya nchi masuala ya Maktaba kwa teknolojia za kisasa ili kutekeleza shughuli za Bodi kwa viwango vya kimataifa kama zilivyo maktaba nyingi za ughaibuni.
Awali katika taarifa yake kuhusu Bodi, majukumu na shughuli inazotekeleza, Mkurugenzi Mkuu wa TLSB Dkt. Mboni Ruzegea, alieleza pia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne (2021 -2025), huku akiipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimairisha miundombinu ya maktaba kwa kujenga na kukarabati majengo ya maktaba nchini, uanzishaji wa Maktaba Mtandao Jumuishi ya Kitaifa, ununzi wa vifaa vya TEHAMA, maboresho ya sheria, ongezeko la Bajeti, ongezeko la Watumishi kupitia ajira mpya na mradi wa ununuzi wa Vitabu vitakazosambazwa kwenye Maktaba za jamii nchini na kuanzishwa kwa kozi mpya chuoni SLADS.
Katika ziara hiyo, Naibu Katibu Mkuu pia alipata wasaa wa kutembelea Divisheni na Vitengo vya TLSB na kufanya kikao na Watumishi wa TLSB.