Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania

TLSB Logo TLSB Logo
Tafuta kwenye kwa
MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA UMAHIRI (LITERACY)
09 Sep, 2025
service image
Jamii imekubushwa kutumia Maktaba kujiongezea maarifa kwani Maktaba ni kitovu cha elimu endelevu na sio ghala la kuhifadhia vitabu pekee. Hayo yamesemwa leo tarehe 9 Septemba 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Maulid H. Dotto na Mgeni Rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Umahiri (Literacy) yaliyofanyika katika viwanja vya Maktaba ya Mkoa wa Morogoro. Mhe. Dotto, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima, amesema ni wakati sasa jamii kurudia utamaduni wa kujisomea kupitia Maktaba kwani kwa kufanya hivyo jamii itapiga hatuna haraka na kujipatia maendeleo kwani Maktaba ni sehemu inayowakutanisha watu wa rika zote. “Tukiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Umahiri hapa Mkoani Morogoro leo, ninawasihi sote tuondoke tukiwa tumepata msukumo wa kuwa mabalozi wa kusoma na kuandika kwani jamii yenye kusoma ni jamii yenye ustawi, na taifa linalosoma ni taifa linaloongoza’’ameeleza Mhe Dotto. Aidha, kulingana na Kauli Mbiu ya Maadhimisho hayo kwa mwaka huu, isemayo ‘Kukuza umahiri katika enzi ya Kidijitali’, Mhe. Dotto ameipongeza Bodi kwa jitihada zake za kutanua wigo wa utoaji huduma za Maktaba kupitia Maktaba Mtandao Jumuishi ya Kitaifa. ‘Bodi imekuwa mstari wa mbele katika kukuza ari ya usomaji na hivyo, uanzishaji wa Maktaba Mtandao Jumuishi ya kitaifa, utawezesha wananchi wa pembezoni mwa miji, kupata taarifa na maarifa kwa wakati sahihi. Ameongeza Mhe. Dotto. Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TLSB Dkt. Mboni Ruzegea amemshukuru Mhe. Dotto kwa kutenga muda wake kushiriki katika Maadhimisho hayo. Katika Hotuba yake, Dkt. Ruzegea amezungumzia ulazima wa mazingira bora ya usomaji shuleni, vipindi vya kujisomea Maktaba za shule, kuhamasisha jamii kujiunga na kutumia huduma za Maktaba. Aidha, amewataka wazazi kuhakikisha watoto wanatumia Maktaba kujisomea badala ya kuangalia runinga, hii itawasaidia kuongeza maarifa. Dkt. Ruzegea metumia jukwaa hilo kuikumbusha jamii umuhimu wa kusikiliza na kuchuja taarifa katika kipindi hiki cha uchaguzi na wasipotoshwe na taarifa wanazozisikia kwani zinaweza kuwa si sahihi. Pichani: (Katikati) Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Maulid H. Dotto, Mgeni Rasmi, akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa TLSB Dkt. Mboni Ruzegea (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Uendeshaji Huduma za Maktaba Dkt. Rehema Ndumbaro (wa kwanza kushoto, Kaimu Afisa Elimu Sekondari Bi. Amna Kova (wa pili kulia) na Mkutubi wa Mkoa wa Morogoro Bi Devota Ndunguru hii leo tarehe 9 Septemba, 2025, katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Umahiri, yaliyofanyika katika viwanja vya Maktaba ya Mkoa wa Morogoro. Sambamba nao (Waliosimama) ni viongozi kutoka TLSB, PATA na Serikali ya mtaa wa Old Dar es Salaam, Morogoro, na picha mbalimbali katika maadhimisho hayo.