MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA UMAHIRI DUNIANI
08 Sep, 2025
MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA UMAHIRI (LITERACY) YAFANA
Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) imeadhimisha Siku ya Kimataifa ya Umahiri (Literacy), leo tarehe 8 Septemba, 2025 katika viwanja vya Maktaba ya Mkoa wa Morogoro.
Katika kuadhimisha siku hii muhimu, Bodi imeandaa maadhiimsho kwa siku mbili mfululizo ambazo ni leo na kesho tarehe 9 Septemba, 2025 ili kuwakutanisha Wadau wa masuala ya Elimu na Maktaba kwa ujumla nchini kuangalia namna bora ya kwenda na kasi na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia.
Hivyo, takribani wanafunzi mia moja (100) wakiongazana na walimu wao, wameshiriki katika maadhimisho haya leo kutoka shule tatu (3) za Mwere ‘A’, Mwere ‘B’ na Mchikichini ‘A’ zote kutoka Wilaya ya Morogoro mjini.
Miongoni mwa shughuli zilizofanyika ni pamoja na wanafunzi kushindana katika kujibu maswali /chemsha bongo hasa kwenye eneo la TEHAMA sawasawa na Kauli Mbiu inavyojitanabaisha.
Vilevile, Mashindano ya kusoma na kuandika Insha, Hadithi, na mashindano ya kuimba ambapo zawadi kwa washindi zitatolewa na Mgeni rasmi katika Hafla Kuu ya Maadhimisho haya itakayofanyika hapo kesho tarehe 9 Septemba, 2025 katika viwanja vya Maktaba ya Mkoa Morogoro, ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima sambamba na Viongozi kutoka Serikalini na Sekta binafsi.
Katika dunia ya sasa, ujuzi wa kidijitali ni sawa na ujuzi wa kusoma na kuandika katika karne zilizopita. Hivyo, unahitajika shuleni, vyuoni, kazini, kwenye biashara na maisha ya kila siku katika kijamii.
Pichani: Mkutubi Mwandamizi Mambo J. Mambo akiongoza sehemu ya maswali/chemsha bongo katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Umahiri leo tarehe 8, Septemba 2025 katika Viwanja vya Maktaba ya Mkoa wa Morogoro.