Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania

TLSB Logo TLSB Logo
Tafuta kwenye kwa
TASNIA YA VITABU YATAJWA KUWA HAZINA YA TAIFA, YATAKIWA KULINDWA KWA GHARAMA ZOTE
26 Nov, 2025
service image
Tasnia ya vitabu nchini inapaswa kulindwa na kutunzwa kwa gharama yeyote ile kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo. Hayo yamesemwa leo tarehe 26 Novemba, 2026 na Mgeni rasmi, ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa TLSB Dkt. Mboni Ruzegea akimwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda katika hafla ya Ufungaji wa Maonesho ya 32 ya Kimataifa ya Vitabu yaliyofanyika katika viwanja vya Maktaba Kuu ya Taifa, Posta Dar es Salaam. "Katika maonesho haya, imedhihirika kuwa vitabu vimesheheni utajiri mkubwa wa maarifa kwa vizazi vya sasa na vijavyo hivyo vinapaswa kutunzwa na kulindwa kwa gharama yeyote ile" amesema Dkt Ruzegea. Pia, ameongeza katika maonesho ya vitabu kwa mwaka huu imedhihirika kuwa hali ya usomaji imeongezeka kufuatia mwitikio wa wananchi waliojitokeaza katika maonesho hayo tangu yalipoanza tarehe 21 Novemba, 2025 hadi leo tarehe 26 Novemba, 2025 ambapo maonesho haya yanatamatika. Aidha, aliongeza kuwa, kwa maonesho yajayo waandaaji waandae ratiba na kuitoa mapema ili Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iweze kushiriki kwenye uandaaji. Vilevile, kufuatia maombi ya Chama cha Wachapishaji Tanzania kupitia Mwenyekiti wake Ndg. Hermes Damian, Dkt. Ruzegea ameahidi kuyawasilisha Wizarani kwa utekelezaji. Awali, akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt. Aneth Komba, ametoa wito kwa Chama cha Wachapishaji Tanzania (PATA) ambao ndio waandaji wa Maonesho hayo, kuendelea kuandaa Maonesho hasa kipindi cha likizo ili wanafunzi wengi waweze kushiriki kwani mtoto anapaswa kujengewa utamaduni wa kujisomea tangu mdogo. Katika hafla ya Ufungaji, Watunzi, wachapaji na wachapishaji wa vitabu walioshiriki maonesho hayo walishindanishwa na washindi kupewa tuzo na vyeti. Maonesho ya 32 ya Kimataifa ya Vitabu yalifunguliwa rasmi tarehe 21 Novemba 2025 na Waziri wa Habari, utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Prof. Palamagamba kabudi na kutamatika leo tarehe 26 Novemba, 2025. Maonesho hayo yalikua na kaulimbiu Vitabu ni hifadhi ya urithi, utamaduni na maarifa na yamehudhuriwa na wachapishaji na waandishi wa vitabu kutoka Afrika Mashariki .