Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania

TLSB Logo TLSB Logo
Tafuta kwenye kwa
MENEJIMENTI YA TLSB NA MAKTABA YA JAMII BUSTANI WAFANYA MAZUNGUMZO KUELEKEA UZINDUZI WA MAKTABA HIYO
04 Aug, 2025
service image
Menejimenti ya TLSB na Uongozi wa  Maktaba ya Jamii Bustani iliyoko Rombo mkoani kilimanjaro, wamekutana leo tarehe 31 Julai, 2025 katika Ukumbi Mkuu wa Mikutano TLSB Dar es salaam, katika kikao maalum cha maandalizi na kujadili mambo kadhaa ikiwemo Mkataba wa makubaliano ya kazi (MoU), ikiwa ni hatua za mwisho kuelekea uzinduzi wa Maktaba hiyo unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni. Akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TLSB, Mkurugenzi wa Uendeshaji Huduma za Maktaba Dkt. Rehema Ndumbaro, ameukaribisha Uongozi wa Maktaba hiyo na kutumia jukwaa hilo kuelezea juhudi za Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia TLSB katika kuanzisha Maktaba za jamii ili kuwafikia umma nchini na kuwawezesha kupata taarifa na maarifa yatakayowasaidia kujikwamua katika nyanja mbalimbali za maisha yao. Aidha, ameeleza kuwa TLSB iko mbioni kuzidundua maktaba za jamii 15 nchini na kusambaza vitabu ambavyo tayari vimeshanunuliwa. "Maktaba ni sehemu muhimu ambapo kunahifadhiwa machapisho na taarifa mbalimbali za kihistoria na tamaduni zetu kwa urithi wa vizazi vya sasa na vijavyo" Hivyo, ameeleza kuwa TLSB itapeleka vitabu na machapisho ili kuongeza nguvu katika maktaba ya Bustani na kutoa mafunzo na ushauri kwa Wakutubi watakao hudumu katika maktaba hiyo. Kwa upande wa Uongozi wa Maktaba ya Bustani ambao ni Ndug. Romani Urassa na Ndug. Fidelis Swai, wameushukuru Uongozi wa TLSB na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa juhudi za kuendelea kuhamasisha utamaduni wa kujisomea ili kuwa na jamii iliyoelimika. Akieleza dhumuni la kuanzisha maktaba ya Jamii Bustani, Ndug. Romani Urassa ameeleza kuwa walipata wazo hilo baada ya kufanya kazi pamoja na ndug. Fidelis Swai na wenzao wawili kwa muda mrefu,  na kugundua jamii inayowazunguka kuwa inahitaji maarifa ili kujikwamua kiuchumi hasa vijana wa kike ambao wakimaliza elimu ya msingi au sekondari huishia kukaa nyumbani na kubaki katika maisha duni. Vilevile, kwa vijana wa kiume ili kuwaepusha na ulevi na michezo ya Kamari, hivyo wakaona ni vyema waanzishe maktaba. Aidha ameeleza kuwa wamefanikiwa kujenga jengo la Maktaba na kituo cha jamii, ambapo mpaka sasa tayari Kompyuta 30 zimeshawekwa.