TLSB YASHIRIKI UZINDUZI WA KITABU “SHE GARAGE”
09 Aug, 2025
Waandishi wa vitabu nchini wametakiwa kuzingatia maudhui yanayoendana na mila, desturi na tamaduni za Kitanzania katika kazi zao za uandishi, ili kukuza utambulisho wa taifa na kuelimisha jamii kupitia maandiko yao.
Hayo yamesemwa leo tarehe 9 Agosti,2025 Dar es salaam na Bi. Nikobiba Kigadye, Msimamizi Mkuu wa Maktaba za Mikoa wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), alipomwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa bodi ya TLSB katika uzinduzi wa kitabu kipya cha "She Garage", kilichoandikwa na Yasinta Wandiba na uzinduzi wake umefanyika makao makuu kwa kushirikiana na TLSB.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Bi. Kigadye amewataka waandishi wote kuhakikisha wanajisajili kwa kupata namba za ISBN (kwa vitabu vya karatasi) na ISSN (Majarida na magazeti), ili kuimarisha urasimishaji wa kazi za fasihi na kuwezesha upatikanaji wake kwa urahisi katika maktaba na soko la kimataifa.
Kitabu cha She Garage kinamwelezea mtoto wa kike aliyekulia kijijini ambaye alipambana kuvuka vizingiti vya kijinsia hadi kuwa mtaalamu wa kutengeneza magari. Yasinta Wandiba, mwandishi wa kitabu hicho, amesema kuwa jamii imekuwa ikiweka mashinikizo mengi kwa mtoto wa kike, jambo linalodhoofisha uwezo wake wa kuchagua mustakabali wake.
"Jamii yetu ina maelekezo mengi kwa mtoto wa kike kuliko wa kiume. Hii imetufanya sana tuweke nguvu zaidi kumtia moyo mtoto wa kike kuwa anaweza kuwa chochote anachotamani kuwa," alisema Yasinta.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Bi. Mercy Mchechu, amesisitiza kuwa wakati umefika kwa jamii, hususan wazazi, kuacha tabia ya kuwachagulia watoto wao michezo kulingana na jinsia.
"Tunapaswa kuacha kuwapa watoto wa kike midoli na wa kiume magari kwa sababu hii hujenga mitazamo inayowabagua watoto katika ndoto zao.Vitabu vina nafasi kubwa katika kubadilisha hali hii kwa kuandika hali halisi ya maisha ya Watanzania ikiwemo miji yetu, vyakula, na tamaduni zetu," alisema Bi. Mercy.
Aidha, ametoa wito kwa waandishi na wachapishaji kuzingatia matumizi ya mbinu shirikishi za kujifunza (interactive learning) kupitia vitabu, ili kuwajengea watoto uelewa mpana wa elimu ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Sanaa na Hesabu (STEAM) tangu wakiwa wadogo.
Uzinduzi wa She Garage ni moja ya jitihada muhimu za kukuza usomaji wa vitabu kwa watoto vyenye maudhui ya kijinsia na kuwawezesha watoto wa kike kujitambua, kujithamini na kujitokeza katika nyanja mbalimbali za kijamii na kitaaluma.