Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania

TLSB Logo TLSB Logo
Tafuta kwenye kwa
WAAJIRIWA WAPYA TLSB WAASWA KUZINGATIA SHERIA NA KANUNI ZA UTUMISHI WA UMMA KATIKA UTUMISHI WAO
08 May, 2025
service image
Waajiriwa wapya wapatao 51 wameaswa kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma ili kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa weledi  na ufanisi. Hayo yamesemwa tarehe 07 Mei, 2025 na Mgeni Rasmi na Mkurugenzi Mkuu wa TLSB Dkt. Mboni Ruzegea katika mafunzo kwa Waajiriwa wapya kazini (Induction training) yanayofanyika katika Ukumbi wa Mikutano ADEM - Bagamoyo, mkoani Pwani. Akifungua mafunzo hayo, Dkt. Ruzegea amewakaribisha na kuwataka Watumishi hao wapya katika Utumishi wa Umma kufuata Sheria,  taratibu na kanuni za Utumishi wa Umma ili wasijiingize matatizoni na hatimaye kupoteza kazi zao. "Hii ni dhamana kubwa mliyopewa na Serikali kuwatumikia wananchi, wapo vijana wengi wenye sifa kama zenu, lakini mpaka sasa bado wanatafuta ajira. Hivyo hii ni nafasi adhimu kwenu mkaitumikie kwa uaminifu na bila manung'uniko" ameeleza Dkt. Ruzegea. Dkt. Ruzegea ameongeza kuwa, mbali na Sheria, Kanuni na taratibu katika utumishi wa umma, Waajiwa hao wanapaswa pia kusoma, kuelewa na kuzingatia Sheria ya TLSB ili kuifahamu Bodi, Majukumu yake na mawanda yake katika kutekeleza majukumu yao. Vilevile ameongeza kuwa, mbali na sheria ya TLSB, wanapaswa kufahamu Muundo wa Bodi, kuanzia ngazi ya juu ambayo ni Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,  Kamishna wa Elimu, Bodi ya Wakurugenzi, Wakuu wa Idara na Vitengo mpaka ngazi za chini kwa watumishi. Aidha, amewataka kufuata utamaduni (Organizational Culture) na thamani (Values) za TLSB ili kuishi kwa amani na kuepusha migogoro kazini. "Kama ilivyo sehemu yeyote ile, TLSB tuna utamaduni wetu na thamani zetu ambazo zinatutofautisha na wengine, hivyo mnapaswa kuishi kwa kufuata utamaduni huo kwani TLSB ni kama Meli kubwa iliyobeba kila mtu na utamaduni wake, lakini mkishakaa ndani yake mnapaswa kuwa na utamaduni mmoja" ameongeza Dkt. Ruzegea. Vilevile amewahimiza kuyajua mazingira yao ya kazi, wadau na wananchi wanaotumia huduma za Maktaba kote nchini ili wawahudumie kwa moyo mkunjufu bila ubaguzi wowote ule. Dkt. Ruzegea alihitimisha kwa kuwataka Waajiriwa wapya kusikiliza kwa umakini na kuuliza maswali ya msingi katika mada zote zitakazowasilishwa na Wakuu wa Idara na Vitengo TLSB, na wawezeshaji kutoka nje. Awali akimkaribisha Mgeni Rasmi na Mkurugenzi Mkuu wa TLSB, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala Bi. Veneranda Mpaze, amemshukuru kwa kuitikia wito wa kufungua mafunzo hayo muhimu katika Utumishi wa umma na kuwataka waajiriwa wapya kujifunza kuhusu dhana ya Utumishi wa Umma, miiko, maadili na taratibu zote za kufuata katika utumishi wao mpaka watakapostaafu. Mafunzo ya awali kwa Waajiriwa wapya TLSB yameanza rasmi tarehe 07 Mei, 2025 na yatatamatika tarehe 09 Mei, 2025.