Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania

TLSB Logo TLSB Logo
Tafuta kwenye kwa
WAANDISHI WA VITABU WAMETAKIWA KUWA WABUNIFU KATIKA UANDISHI WAO
24 Nov, 2025
service image
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, amewataka waandishi wa vitabu nchini kuwa wabunifu katika kazi zao ili kuongeza hamasa ya usomaji na kudumisha amani na umoja wa Watanzania. Profesa Kabudi ametoa wito huo jijini Dar es Salaam leo tarehe 21 Novemba, 2025 wakati akifungua Maonesho ya 32 ya Kimataifa ya Vitabu Tanzania. “Tasnia ya uandishi wa vitabu ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kuhifadhi utamaduni, uandishi unaozingatia ubunifu huongeza hamasa kwa wasomaji pamoja na kujenga uzalendo, uwezo wa kutafakari, kujiamini na kutoendeshwa na mkumbo” amesema Prof. Kabudi. Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania, Dkt. Mboni Ruzegea, amesema kuwa katika juhudi za kukuza usomaji wa vitabu vya ndani, serikali imeanza kuimarisha maktaba za jamii na maktaba mtandao, pamoja na kuanza ununuzi wa vitabu kutoka kwa waandishi wa ndani. Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wachapishaji wa Vitabu Tanzania (PATA), ndug. Hermes Damian, amesema sekta ya uandishi wa vitabu bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali za kisera na kimiongozo. Aidha, Mjumbe wa Bodi kutoka Chama cha Wachapishaji nchini Kenya ndug. Musyoki Muli amependekeza kuanzishwa kwa maonesho ya uandishi wa vitabu Afrika Mashariki ili kukuza tasnia hiyo kwa kiwango cha kikanda. Maonesho ya 32 ya Kimataifa ya Vitabu Tanzania yatafanyika kwa siku sita kuanzia Novemba 21 hadi 26, yakiwa na kaulimbiu “Vitabu ni hifadhi ya maarifa na utamaduni”. Maonesho hayo yanawahusisha waandishi wa vitabu, wachapishaji, wasomaji na wadau mbalimbali wa sekta ya elimu na utamaduni.