Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania

TLSB Logo TLSB Logo
Tafuta kwenye kwa
WANAFUNZI WA SHULE YA MSINGI ULONGONI ‘A’ WATEMBELEA MAKTABA YA TAIFA
18 Oct, 2025
service image
Wanafunzi 102 wa Shule ya Msingi Ulongoni ‘A’ kutoka Manispaa ya Ilala, mkoani Dar es Salaam, wametembelea Maktaba ya Taifa Posta kwa lengo la kujifunza kwa vitendo historia ya Tanzania kupitia  vitabu,machapisho na picha za viongozi zilizohifadhiwa katika Maktaba leo tarehe 17 Oktoba,2025 . Wanafunzi hao walipokelewa na Mkuu wa Kitengo cha Watoto (CSSD), Bi. Mwajuma Rasuli, pamoja na Wakutubi wengine wa kitengo hicho, aliwakaribisha wanafunzi na kuanza ziara kwa kutembelea kitengo cha Ufundi (TSD) kinajishughulisha na uandaaji, uagizaji, utayarishaji na usambazaji wa machapisho katika Maktaba, Kisha walienda Kitengo  cha Usomaji Watu Wazima (RSD) ambapo walipewa elimu ya Maktaba na kuoneshwa vitabu vya kihistoria,hadithi na picha za viongozi mbalimbali vilevile waliwaelezwa kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na kitengo cha watoto, ikiwemo kusoma, kuazima vitabu, na kujifunza mbinu za uandishi na ubunifu. “Maktaba ni hazina ya maarifa. Tunawahimiza wazazi na walimu kuwaleta watoto maktaba mara kwa mara ili wasome na kuazima vitabu, jambo litakalowasaidia kuongeza maarifa na kukuza uwezo wa kufikiri kwa kina,” alisema Bi. Mwajuma. Kwa upande wake Bw. Amir Amir, Mkutubi kutoka Kitengo cha Watoto, aliwaongoza wanafunzi kwenye shughuli ya ubunifu ya kuandika hadithi yenye kichwa “Hadithi ya Hadithi Yangu”. Wanafunzi waliandika kuhusu vitu walivyoviona na kuvipenda zaidi ndani ya maktaba, pamoja na yale wasiyoyapenda, katika karatasi maalum alizowagawia. Zoezi hilo lilifanyika katika makundi 10 lililenga kukuza fikra bunifu (critical thinking) na ushirikishwaji wa maarifa (knowledge sharing) miongoni mwa wanafunzi ikiwemo kuwa  na uhuru wa kujieleza. Naye kiongozi wa msafara huo, Mwl. Mustafa Semkiwa, alisema kuwa ziara hiyo imelenga kuwasaidia wanafunzi kujifunza kwa vitendo historia ya nchi sambamba na kuhamasisha utamaduni wa kusoma. “Tunatambua umuhimu wa elimu ya vitendo kwa wanafunzi wetu. Kupitia ziara hii, tunawapa fursa ya kuona vitabu mbalimbali vya historia na picha ya viongozi kabla na baada ya Uhuru vilivyohifhadhiwa ndani ya Maktaba kuu ya Taifa.,” alisema Mwalimu Semkiwa. Vilevile  Mwl. Josephine Niontimba,ambaye ni  mwalimu wa somo la Maarifa ya Jamii na msimamizi wa ziara hiyo, alisema kuwa ziara hiyo ni maalum kwa wanafunzi wa darasa la tano kutembelea maktaba, hatua inayolenga kuimarisha uelewa wa masomo na kuijua Historia ya nchi kupitia vitabu. “Hata hivyo katika somo la Kiswahili kuna kipengele cha Maktaba kinachowasaidia wanafunzi kujifunza taratibu za usomaji na upangaji wa vitabu. Ziara kama hizi zinawawezesha wanafunzi kuunganisha nadharia na vitendo,” alifafanua Mwl. Josephine. Aidha jumla ya wanafunzi 102 wa darasa la tano walishiriki katika ziara hiyo, wakiwa wameambatana na walimu sita kutoka shule Ulongoni ‘A.’